Aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya
Jiji la Arusha, Raphael Mbunda (51) na wenzake watatu, wamefikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na kusomewa shitaka la kuhujumu
uchumi, kwa kutumia vibaya madaraka yao na kuisababishia hasara serikali
baada ya kuipatia tenda, kampuni ya Luneco Investment Company Limited,
kinyume cha sheria.
Washitakiwa wengine ni aliyekuwa
Mweka hazina wa Manispaa hiyo, Christopher Mbalakai (37), Mwansheria wa
Manispaa hiyo, Paulo Mugasha (45) na Mkurugenzi wa kampuni ya Luneco
Investment Company Limited, Nestory Ng’hoboko.
Akisoma mashitaka hayo mwendesha
mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Hangi
Chang’ah , mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Gantwa Mwanguga, alidai
kuwa washtakiwa hao wameshitakiwa kwa makosa manne, ambapo shitaka la
kwanza hadi la tatu linawahusu washitakiwa watatu tu.
Mwendesha mashitaka huyo alisema
shitaka la kwanza Mkurugenzi huyo na wenzake ambao ni mweka hazina na
mwanasheria, wanashitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka, kati ya
mwaka 2008 na 2010 kwa siku toauti, kwa kumkaribisha mdhabuni wa kampuni
ya Luneco Investment Company Limited bila kufuata taratibu za utoaji
tenda na kuvunja sheria.
Shitaka la pili ilidaiwa kuwa
washitakiwa hao wanashitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka
waliyofanya Agosti 23 mwaka 2010 kwa kuruhusu tenda kwa kampuni hiyo ya
kukarabati eneo la maegesho ya magari na bustani huko Kijenge manisapaa
ya Arusha, kinyume cha sheria.
Chang’a alisema kuwa shitaka la
tatu washitakiwa hao, walitenda kosa lingine Agosti 23 mwaka 2010 kwa
kuipatia kazi kampuni ya Luneco Investment Company Limited ambaye
alijiptia sh milioni 45.7 wakati hakustahili kuzipata.
Shitaka la nne lilisomwa kwa
washitakiwa wote wanne, ambapo ilidaiwa walitenda kosa Agosti 23, 2010
na Septemba 2010, walishindwa kusimamia kazi hiyo na kusababishia
serikali hasara ya Sh milioni 25.5.
Washitakiwa wote walikana mashitaka
hayo na wako nje kwa dhamana, ambapo kila mshitakiwa alitakiwa kuwa na
mdhamini mmoja mwenye mali ya shilingi milioni tano na kitambulisho na
mshitakiwa wanne alitakiwa kuwa na mdhamini mwenye mali isiyohamishika
ya shilingi milioni tano na alitimisha masharti hayo na wote wapo nje
kwa dhamana hadi kesi itakapotajwa tena Julai 19 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment