NEWZ:Dalili za kuanza mgawo wa umeme zadhihirika





Kuna hatari ya taifa kuingia tena katika makali ya mgawo wa umeme kutokana na kina cha maji kinachotumika kuzalisha nishati hiyo katika Bwawa la Mtera kupungua kwa kasi kutoka ujazo mita 8.5 hadi kufikia mita 1.2 kiwango ambacho kinakaribia kulilazimisha Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuwasha mitambo yake ya kuzalisha nishati hiyo kwa ratiba.

Tanesco wametaja sababu kubwa iliyosababisha kuwapo kwa hali hiyo ya kupungua kwa maji katika bwawa hilo kwamba kinasababishwa na matumizi mabaya ya maji yanayofanywa na wakulima wa kilimo cha umwagiliaji wa zao la mpunga katika tarafa ya Pawaga, wakulima wa vijiji vinavyolizunguka bwawa hilo pamoja na wafugaji ambao wanaharibu vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji hayo kwenda bwawa la Mtera kwa kulisha mifugo yao.

Tahadhari hiyo imetolewa na Meneja wa Tanesco anayesimamia uzalishaji wa umeme katika bwawa hilo, Mhandisi Anthony Mbushi wakati akijibu maswali mbalimbali ya wadau wa bwawa hilo katika mkutano wa wadau wa ardhi oevu, waliokuwa wakijadili changamoto zinazolikabili bwawa la Mtera katika Kijiji cha Migoli hivi karibuni.

"Ndugu zangu hii ni hatari ingawa pia hata watu wa Bonde la mto Rufiji (PBWO) tumewapa taarifa kuhusu hali hiyo...Kwa hali ilivyo tunalazimika kutumia maji kwa ungalifu zaidi maana tunaogopa yakipungua zaidi ya hapo tunarudi kule kule kwenye mgawo," alisema Mbushi.

Kutokana na kujitokeza kwa hali hiyo, mmoja wa wadau hao, Allan Mbilinyi, ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mtera, alisema licha ya wananchi wanaolizunguka bwawa hilo kuhamasishwa kuhifadhi mazingira na kuvilinda vyanzo vya maji kwa lengo la kulinusuru kukauka, kuna tatizo la kisera ambalo linawafanya wananchi wa Wilaya za Mpwapwa na Chamwino mkoani Dodoma kuona juhudi zinazofanyika kulinusuru bwawa hilo kama haziwahusu licha ya kwamba na wao ni watumiaji wakubwa wa bwawa hilo.

"Sisi hapa tunajitahidi sana hadi tumeanzisha vikundi vya kusimamia na kudhibiti uvuvi haramu maarufu kama BMU's ambavyo kimsingi viliundwa chini ya mradi wa SWMP unaotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vijijini kwa ufadhili wa DANIDA lakini wenzetu wa upande wa Dodoma wao wanafanya hata yale yasiyoruhusiwa ikiwamo matumizi ya maji yasiyofuata njia salama ya uhifadhi," alisema Mbilinyi.

Prosper Njau, Mratibu wa Mradi wa Maeneo Oevu katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, akiwasilisha taarifa yake katika mkutano huo wa wadau wanaotumia maji ya bwawa la Mtera, alisema kwa kuwa mradi huo unatekelezwa katika vijiji 15 vya Wilaya ya Iringa iko haja kwa serikali kuandaa maeneo maalumu ya wafugaji ambao kwa sasa wamo hata kando kando ya bwawa la Mtera kuondoka eneo hilo kwa lengo la kunusuru vyanzo vya maji.

Katika hatua nyingine, Kaimu Afisa wa Bonde la Mto Rufiji (RBWO), Grace Chitanda, alitangaza vita na wananchi waliojenga makazi yao na kuendesha shughuli za kiuchumi kando kando ya bwawa hilo kuondoka mara moja, kwa kuwa serikali haitakuwa na chakusubiri zaidi ya kubomoa nyumba za makazi na nyumba za biashara au ofisi zilizopo mita 500 kutoka katika bwawa la Mtera.

Hata hivyo, taarifa zilizolifikia NIPASHE jana zinasema kuwa maofisa wa bonde hilo la mto Rufiji tayari wamekwishaweka alama za X katika nyumba za makazi, maeneo ya biashara, shule na baadhi ya misingi ya nyumba ambazo zinakusudiwa kujengwa kwa lengo la kulinda hifadhi ya bwawa la Mtera ambalo limeathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kiuchumi.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment