DODOMA.
Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ya sh trilioni 15
iliyokuwa ikipingwa na wabunge wengi Ijumaa ya Juni 22, 2012 ilipita
kwa kura 225 za ndiyo na 72 za hapana, huku baadhi ya wabunge wa chama
tawala wakiungana na wapinzani kuikataa.
Aliye ongoza
wabunge wa CCM alikuwa mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, ambaye
alishikilia msimamo wake wa kuipinga na kuamua kutoka nje ya ukumbi
wakati wa kupitisha.
Mbali na
Mpina wabunge wengine wawili wa CCM, Kangi Lugora (Mwibara) na Deo
Filikunjombe (Ludewa) ambao waliikosoa vikali bajeti hiyo nao walikwepa
upigaji kura kwa kutofika kabisa ukumbini.
Mpina
aliikataa waziwazi bajeti hiyo mara baada ya kuwasilishwa bungeni na
hata wakati alipochangia juzi, alisema kuwa inakinzana na Mpango wa
Maendeleo wa Taifa.
Muda mfupi
kabla ya upigaji kura kuanza, mawaziri William Lukuvi na Stephen
Wassira, walionekana wakihaha kumshawishi mbunge huyo bila mafanikio.
Wakati Mpina
akiwa nje na jina kutajwa mara mbili bila kuitikia, wabunge wote wa
kambi ya upinzani walimshangilia kwa kupiga makofi.
Akizungumza
nje ya ukumbi wa Bunge, Mpina alisema anayo mambo mengi ya kusema kuhusu
bajeti hiyo aliyoikataa tangu awali na kusisitiza.
Vilevile
wabunge wote wa kambi ya upinzani walipiga kura ya hapana isipokuwa
mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), pekee ndiye aliyeunga
mkono bajeti hiyo.
Pia mbunge
wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, alishangiliwa kwa nguvu na wapinzani baada ya kuitwa jina
na kusema hapana.
Akitangaza
matokeo hayo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema: “Idadi ya
wabunge inapaswa kuwa 357 lakini waliopo ni 351 na waliopiga kura ni
297 ambapo kura za ndiyo ni 225 na hapana ni kura 72.”
Baada ya
hapa Spika Makinda alitangaza kuwa waliopiga kura ya ndiyo wameshinda na
hivyo bajeti hiyo imepita, lakini akawapongeza wabunge wote kwa pamoja
akisema wamefanya kazi nzuri licha ya kusigana katika hoja.
“Waheshimiwa
wabunge nawapongeza sana kwa kazi kubwa, lakini muelewe kuwa
kutofautiana kifikra kwa Bunge kama hili si jambo baya ni kulenga
kuwatetea wale waliowatuma,” alisema.
Wakizungumza
baada ya Bunge kuahirishwa, baadhi ya wabunge Tundu Lissu (Singida
Mashariki), Mbatia na Cecilia Paresso (Viti Maalum), walisema waliikataa
bajeti kwa kuwa haina jipya.
“Bajeti ni ile ile na wabunge wa CCM ni wataka maslahi wala hawako kwa ajili ya kuwatetea wananchi,” alisema Lissu.
Naye Mbatia,
alisema kuwa bajeti haijafafanua mgawanyo halisi wa fedha na kwamba
serikali imeshindwa kuonyesha ni namna gani itadhibiti mapato
yanayopotea.
“Mathalani
jijini Dar es Salaam, serikali inapoteza sh bilioni nne kutokana na
msongamano wa magari, watu wanapoteza muda mwingi bila kufanya kazi
lakini bajeti haisemi ni hatua gani zinachukuliwa,” alisema.
Aliongeza
kuwa hata kauli ya waziri kuwa serikali inayapokea maoni ya wapinzani
kwa ajili ya kuyafanyia kazi ni hadaa inayofanyika miaka yote.
Kwa upande
wake Paresso, alisema kuwa bajeti hiyo haijaeleza wazi ni kwa namna gani
serikali itawawezesha vijana kupata mikopo ili waweze kuwekeza katika
ujasiriamali.
No comments:
Post a Comment