Mgonjwa
akiwa nje ya geti la Taasisi ya Mifupa MOI jijini Dar es Salaam jana
akiwa ajui chakufanya baada kukuta geti hilo limefungwa kutokana na
mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.Picha na Venance Nestory
MADAKTARI
146 wamefukuzwa katika hospitali mbalimbali nchini kutokana na
kushiriki mgomo unaoendelea nchi nzima kwa lengo la kuishinikiza
Serikali kutekeleza madai yao.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini
kuwa, madaktari hao walitimuliwa katika Hospitali za Bugando na Sekou
Toure mkoani Mwanza na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na ile ya
Rufaa Dodoma.
Wakati Serikali ikichukua hatua hiyo, mgomo huo
jana uliendelea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Ocean Road,
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) za jijini Dar es Salaam, Hospitali ya
Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
Katika
kile kinachoonekana kuwaunga mkono wenzao, madaktari bingwa wa MOI, MNH
na Ocean Road jijini Dar es Salaam, jana walitangaza rasmi kuingia
kwenye mgomo huo hadi madai hayo yatekelezwe.
Madai ya madaktari
ni hali bora ya mazingira ya utoaji huduma nchini, ongezeko la
mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu, posho za
kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa kazini.
Tamko
la madaktari hao bingwa, lilitolewa jana na msemaji wao, Dk Catherine
Mng'ong'o muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao chao kilichofanyika
jijini Dar es Salaam.
Tamko hilo limekuja siku moja baada ya
baadhi yao kuanza kushiriki mgomo huo juzi, kushinikiza pamoja na mambo
mengine, Serikali itoe tamko juu ya tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa
Dk Ulimboka.
Hata hivyo, wakati madaktari hao wakitoa tamko hilo,
uongozi wa Moi jana ulitoa tangazo kuwataka madaktari wote walioshiriki
mgomo huo kurejea kazini ifikapo Julai 2, mwaka huu, vinginevyo
watafukuzwa kazi.
Jana jengo la MOI lilikuwa limefungwa kwa
makufuli, huku wagonjwa wakielezwa kuwa huduma zote hazitolewi zikiwamo
za dharura ambazo awali ziliendelea kutolewa.
Mmoja wa walinzi aliwambia waandishi wa habari kuwa, amefunga mageti kutokana na amri ya mkuu wake wa kazi.
“Mimi
ninatekeleza amri ya bosi wangu, amenitaka kufunga geti na hakuna mtu
kuingia, awe mgonjwa au ninyi waandishi wa habari kwa kuwa hakuna huduma
zinazotolewa humu,” alisema.
Mkoani Mwanza
Madaktari 63 walio
katika mafunzo ya vitendo kazini wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando,
Hospitali ya Mkoa Sekou Toure wametimuliwa na kurejeshwa wizarani
kutokana na mgomo huo.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya
Bugando, Dk Charles Majinge alisema kuwa, juzi aliwataka madaktari
waliokuwa katika mgomo kurejea kazini, lakini hawakufanya hivyo na jana
akaamua kuwarejesha 47 wizarani.
Katika Hospitali hiyo ya Mkoa wa
Mwanza Sekou Toure, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Valentino Bangi alisema,
madaktari 16 wamesimamishwa kufanya kazi kutokana na agizo la wizara.
Kilimanjaro
Madaktari
walioko kwenye mgomo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi mkoani
Kilimanjaro walisema jana kuwa, kinachofanywa na Serikali kuwafukuza
kazi waliogoma, ni njia mojawapo ya vitisho, lakini wakasema kuwa kamwe
hawataogopa.
Madaktari hao ambao hawakutaka majina yao yaandikwe
gazetini walisema, wao wanaendelea na mgomo mpaka pale Serikali
itakapotekeleza madai yao.
“Tumesikia wenzetu wa Dodoma na Mbeya
wamefukuzwa ….Hiyo haitufanyi turudi kazini na kama Serikali inaona hiyo
ndiyo njia ya kumaliza mgogoro huu waendelee sisi tutarudi kazini pale
itakapotimiza tunayotaka,” alisema mmoja wa madaktari hao.
Mbeya
Juzi
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, ilitoa tangazo la kuwataka madaktari
waliopo mafunzoni waliogoma kurejea kazini jana, na endapo wangekiuka
agizo hilo wangekuwa wamejifukuzisha kazi. Na hadi jana jioni hospitali
hiyo ilikuwa imewafukuza madaktari 72.
Ocean Road
Katika
Taasisi ya Taifa ya Saratani, (Ocean Road), kutokana na madaktari sita
kusitisha kutoa huduma tangu Dk Ulimboka alipojeruhiwa kwa kipigo,
waligoma na jana Mkurugenzi wa Tiba na Huduma Diwani Musemo alionekana
akitembelea wagonjwa.
Dodoma
Madaktari 11 wa mafunzo kwa
vitendo katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma nao wamefukuzwa, tukio ambalo
jana lilileta usumbufu mkubwa katika upatikanaji wa tiba hospitalini
hapo.
“Kwa hakika matibabu yanaendelea ingawa ni katika hali ya
kusuasua. Hatuna uhakika kama kweli kuna mgomo wa chinichini au la,
maana mimi nimefika mapema, lakini bado sijahudumiwa," alisema mmoja wa
wagonjwa waliozungumza na mwandishi wa habari.
Arusha
Katika
Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, huduma zimedorora lakini
Mganga Mkuu, Dk Omar Chande alisema jana kuwa, imekuwa ni vigumu
kuchukua hatua kuwabana madaktari ambao wanatuhumiwa kufanya mgomo
baridi, kwani wote wanaripoti kazini.
"Ni kweli kuna taarifa hizi
za kuwapo mgomo baridi, lakini madaktari wote wapo kazini, ila kama
kuna kufanya kazi chini ya kiwango, tumeanza uchunguzi," alisema Dk
Chande.
Amana
Katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam
utoaji wa huduma ulisuasua kutokana na mgomo huo jambo lililofanya
uongozi kuweka tangazo kwenye Ofisi ya Mganga Mkuu kuwataka watumishi
wote ambao hawakuwapo kazini kuanzia Juni 25, 2012 waandike barua za
kurejea kazini.
Tangazo hilo pia linawataka madaktari walioko
mafunzoni kuandike barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kupitia kwa mganga mkuu wa hospitali hiyo.
Habari
hii imeandaliwa na Frederick Katulanda, Mwanza, Rehema Matowo, Moshi,
Zakhia Abdallah (SJMC), Editha Majura, Israel Mgussi, Dodoma), Victoria
Mhagama na Daniel Mwingira, Sam Jacob na Issa lazaro (SJMC, Godfrey
Kahango, Mbeya, na Mussa Juma, Arusha.