TENNIS:ANDY MURRAY AINGIA FAINALI WIMBLEDON.




Andy Murray alionyesha nia ya kufuzu kucheza fainali ya Wimbledon kwa kucheza kwa bidii mno, na kufanikiwa kuwa Muingereza wa kwanza katika kipindi cha miaka 74 kuingia fainali ya mashindano hayo, baada ya kumshinda Mfaransa Jo-Wilfried Tsonga katika nusu fainali.
Murray, mwenye umri wa miaka 25, na ambaye yumo katika nafasi ya nne katika orodha ya wachezaji bora zaidi wa kiume duniani, amefanikiwa kutimiza wajibu ambao wachezaji 11 waliomtangulia wameshinda kukamilisha, tangu Bunny Austin kufika fainali mwaka 1938.
Murray alimshinda Tsonga 6-3 6-4 3-6 7-5 katika muda wa saa 2 dakika 47, na siku ya Jumapili atapambana na Roger Federer kutoka Uswisi, ambaye ni mshindi wa mashindano makubwa ya Grand Slam mara 16.
Hakuna Muingereza ambaye amewahi kuchukua taji kubwa tangu Fred Perry alipofanikiwa kufanya hivyo mwaka 1936.
Perry aliibuka bingwa katika mashindano ya US Open mwaka huo.
Hii ni mara ya nne kwa Murray kuingia fainali ya mashindano makubwa ya Grand Slam, lakini atakuwa na kazi ngumu wakati Federer naye atakuwa anatafuta taji lake la saba.
Lakini licha ya kutazamia upinzani mkali kutoka kwa raia huyo wa Uswisi, Murray pia atahisi ushindi wake utakuwa ni muhimu sana kwa taifa la Uingereza.
"Ninahisi kama nimeutua mzigo, na vile vile nina msisimko, ni vigumu kueleza," alisema mchezaji huyo kutoka Uskochi, alipokuwa akizungumza na BBC Michezo.
"Hatimaye lilikuwa pambano kali, na wote tulikuwa na nafasi ya kupata ushindi.
“Ni muhimu kuwa mtulivu, lakini sio rahisi. Kuna shinikizo nyingi unapokuwa uwanjani, lakini lazima uwe na azma ya kufaulu.”
Kufuatia kushindwa na Andy Roddick mwaka 2009 na Rafael Nadal mwaka 2010 na vile vile mwaka 2011, Murray alifahamu vyema mwaka huu ana nafasi nzuri zaidi ya kufika fainali.
Murray alikuwa amemshinda Tsonga katika mapambano matano kati ya sita ambayo wamekutana, ikiwa ni pamoja na robo fainali ya mwaka 2009, na vile vile pambano la Championship katika klabu ya Queens mjini London.

No comments:

Post a Comment