NEWZ:Vigezo vipya vya kukopesha wanafunzi wa juu kupelekwa bungeni





WIZARA Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema inajiandaa kupeleka bungeni vigezo vipya vya kukopesha wanafunzi wa elimu ya juu ambavyo vinatarajiwa kuanza kutumika mwaka huu wa fedha.
Hayo yalielezwa jana mjini hapa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Mulugo Wakati akijibu swali la mbunge wa Chwaka Yahya Kassim Issa (CCM) aliyetaka kujua suala la upatikanaji wa mikopo namna linavyokwenda kwa kuwa linaonekana kutolewa kwa ubaguzi na kujuana.
Akijibu swali hilo Mulugo alisema tayari wizara yake ilishavifanyia mabadiliko vigezo hivyo na tayari ilishaviwasilisha kwenye Kamati ya Maendeleo ya Jamii chini ya uongozi wa mwenyekiti wake Margareth Sitta.
Alisema suala hilo halina upendeleo hata kidogo na kwamba vigezo vinavyotumika vipo wazi kwa kila mtu na tayari vimeshafanyiwa mabadiliko kama walivyoagiza waheshimiwa wabunge.
Katika swali la msingi mbunge wa Baraza la Wawakilishi Jaku Hashimu Ayoub alitaka kujua ni vigezo gani muhimu vimetumika kujenga vyuo vikuu vyote vya taifa upande mmoja wa Muungano wakati elimu ndio msingi mkuu wa maendeleo ya wananchi wake.
Mulugo alisema vyuo vikuu havianzishwi kwa maana ya kuongeza idadi bali kwa madhumuni maalum kutegemea mahitaji halisi, uwezo wa kifedha wa serikali lakini kwa kiasi kikubwa unategemea sekta binafsi ambayo imetoa mchango mkubwa katika ukuzaji wa elimu ya juu pande zote za Muungano.
Aidha alisema uanzishwaji wa vyuo unategemea uwepo wa wadau wakiwemo wanafunzi wenye sifa, rasilimali watu, mtaji, wahadhiri, miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunza pamoja na madhumuni halisi ya kuanzisha Chuo Kikuu husika.

No comments:

Post a Comment