Na Gabriel Mushi, Gabriel Masese via gazeti la MTANZANIA
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dkt. Stephen Ulimboka,
amesema anatarajia kuanika madudu ya watu waliomteka na kumfanyia
vitendo vya kinyama, baada ya kufanya uchambuzi wa kina mkasa
uliomkumba.
Akizungumza katika mahojiano maalum na MTANZANIA mjini Dar es Salaam
jana, Dkt. Ulimboka alisema ataanika madudu yote aliyofanyiwa, baada ya
siku 40.
Dkt. Ulimboka, aliyerejea kutoka nchini Afrika Kusini, alikokuwa
amekwenda kutibiwa, alisema ana siri nzito moyoni ambayo akiitoa,
Watanzania watamuelewa tu.
Alisema baada ya kurudi nyumbani salama, hivi sasa amejikita zaidi
kufanya uchambuzi wa mambo au matukio yaliyomsibu kabla ya kupelekwa
Afrika Kusini ili ukweli ujulikane.
“Nawaomba Watanzania wawe na subira kwanza, nitaanika kila kitu baada
ya siku 40 kuanzia sasa, jambo kubwa ninaloangalia sasa ni kuimarisha
kwanza afya yangu ambayo Mungu amenipigania vya kutosha, baada ya hapo
nitaeleza kwa kina mkasa huu ulionikuta wakati wa mapambano ambayo nyote
mnayajua. Napenda kuwahakikishia Watanzania na madaktari wenzangu, kuwa
nitaendelea kusimamia kile ninachoamini na kukitetea…nitaendelea
kuongoza Jumuiya ya madaktari, nitaendelea kujiamini ili kuhakikisha
tunapigania madai yetu,” alisema Dkt. Ulimboka.
Kuhusu familia yake, kama inaweza kutoa tamko, Dkt. Ulimboka alisema
hafahamu iwapo familia imeandaa mpango huo, lakini kwa upande wake,
wakati ukifika atalitoa mbele ya umma kama ilivyo kawaida yake kwa
ushahidi wa kutosha, “Kuhusu suala la uchunguzi, siwezi kulizungumzia
sana kwa sababu kama nilivyosema siwezi kukurupuka kuanza kutoa
ushirikiano na Jeshi la Polisi, wakati sijausoma mkasa wenyewe kama
unaendelea vipi. Nimesikia baadhi ya vyombo vya habari, vikisema
nimefichwa, jamani sijafichwa na familia…. naendelea na shughuli zangu
kama kawaida, lakini jambo la msingi ni kuimarisha kwanza afya yangu,
kabla ya kuanza kukutana na waandishi wa habari hadharani,” alisema Dkt.
Ulimboka na kuongeza, “Nipo kwenye mihangaiko yangu na muda huu nipo
safarini, naelekea mjini Bagamoyo.”
Katika hatua ya kushangaza, Dkt. Ulimboka aliamua kutumia usafiri wa
boti kwenda Bagamoyo, tofauti na siku ambazo amekuwa akitumia njia ya
barabara.
Hii ni mara ya kwanza Dk. Ulimboka kuzungumza kwa kina na MTANZANIA,
tangu aliporejea kutoka nchini Afrika Kusini, ambako alikwenda kutibiwa
Juni 27, mwaka huu.
Wakati Dkt. Ulimboka akisema hayo, ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi
nchini, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, aliiambia
MTANZANIA kuwa, hivi sasa jeshi hilo linaendelea na vikao ili kuona ni
namna gani wanaweza kushughulikia suala la Dkt. Ulimboka.
Habari za kuaminika kutoka kwa ofisa huyo, ni kwamba Ijumaa wiki hii
linaweza kutoa ufafanuzi zaidi au hatua zitakazochukuliwa dhidi ya
daktari huyo
No comments:
Post a Comment