Matonya 'ombamba' afariki dunia




Yule ombamba maarufu kuliko wote nchini , Matonya amefariki duniani.

“Namtaarifu Komredi Yusufu Makamba, kuwa yule kiboko yake 'MATONYA' amefariki usiku wa kuamkia juzi kijijini kwakwe Mpamantwa wilaya ya Bahi, mazishi yatafanyika leo saa 10 jioni kijijini hapo. Habari ziwafikie, Mkuu wa Wilaya Betty Mkwasa, Familia ya Mzee Makamba popote walipo, wakazi wa Dar na Moro pamoja na ndugu jamaa na marafiki wote. Bila ya kusahau wale wa eneo la Darajani Mjini Morogoro", ameandika mwandishi wa habari Habel Chidawali ambaye amewahi kumfanyia mahojiano ombamba huyo.

Matonya amefariki akiwa anaishi kwenye nyumba ya tembe ambayo ni mali  ya mtoto wake wa kike aitwaye Elizabeth Matonya.

Nyumba hiyo ya asili ya watu wa Dodoma ipo kwenye Kijiji cha Bahi Sokoni katika Kitongoji cha Nghungugu, umbali wa kilomita 3 kutoka yalipo makao makuu ya wilaya ya Bahi.

Katika mahojiano aliyofanya na Habel, Matinya enzi za uhai wake alisema kuwa hana mali yoyote kama wengi walivyokuwa wanadhani.

“Watu wanasema kuwa nina mali, lakini ni ‘walambi’ (akimaanisha kwamba ni waongo). Mimi sina kabisa mali; hata mbuzi; hata kuku sina na wala sina mpango wa kununua tena hata kama nina pesa kwa kuwa walishazoea kuniibia, hivyo sitaki tena kuwa na mali.”

Nilikuwa na ng’ombe wengi sana. Kila wakati walikuwa wakiwaiba wakati ninaishi Kilimatinde na ng’ombe hao nilinunua kwa pesa yangu ya kuomba huko Dar es Salaam. Walikuwa wengi lakini waliibwa wote na ndugu zangu.

Kuhusu kuacha kuomba

Jibu: Labla serikali inijengee nyumba nzuri hapa na inipe mtu wa kunitunza au hata wakijenga nyumba nzuri kwa mtoto wangu halafu wanisaidie na chakula pamoja na chai ya kila siku, mimi naweza kustaafu kazi yangu lakini bila ya kufanya hivyo kazi yangu nitakufa nayo.

Katika mahojiano hayo Matonya alisema alikuwa akipata kati ya Sh50,000 hadi 100,000 kwa mwezi na mara nyingi alikuwa akirudi kijijini kila baada ya miezi miwili au mitatu tangu alipoanz`a kazi hiyo mwaka 1961.

No comments:

Post a Comment